NGUZO MUHIMU KATIKA BIASHARA YOYOTE.
Utangulizi
Katika ulimwengu wa sasa biashara mpya nyingi huanzishwa kila Siku, kila wiki, kila mwaka. Huku biashara nyingi zinaendelea kuanzishwa, zipo pia biashara nyingi nyingine zikifungwa au kufa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: usimamizi mbovu, ukosefu wa elimu ya pesa na biashara, kufilisika, madeni kutoka taasisi za kifedha, wizi, majanga ya asili, kuendesha biashara kwa hasara bila kujua n.k. Biashara yoyote inategemea wateja ili iendelee kukua. Biashara yoyote ina hitaji usimamizi mzuri, biashara yoyote inahitaji uendeshaji mzuri.
Utangulizi
Katika ulimwengu wa sasa biashara mpya nyingi huanzishwa kila Siku, kila wiki, kila mwaka. Huku biashara nyingi zinaendelea kuanzishwa, zipo pia biashara nyingi nyingine zikifungwa au kufa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: usimamizi mbovu, ukosefu wa elimu ya pesa na biashara, kufilisika, madeni kutoka taasisi za kifedha, wizi, majanga ya asili, kuendesha biashara kwa hasara bila kujua n.k. Biashara yoyote inategemea wateja ili iendelee kukua. Biashara yoyote ina hitaji usimamizi mzuri, biashara yoyote inahitaji uendeshaji mzuri.
Nguzo 8 muhimu.
Kuanzisha biashara na kuhakikisha biashara yako inakua ni mkururo au mfululizo wa mambo mengi muhimu ambayo mafanyabiashara lazima azingatie. Hapa chini nitaelezea mambo kumi (8) muhimu katika biashara:
- Nidhamu binafsi katika biashara.
- Uthubutu katika biashara.
- Uvumilivu mkubwa hasa biashara inapopitia changamoto.
- Utambuzi wa hali ya juu kuhusu uendeshaji wa biashara.
- Kujua namna ya kuongeza wateja wapya na kulinda wateja.
- Kujiwekea malengo katika biashara yako.
- Kuwa mbunifu na kutafuta kujifunza zaidi kuhusu biashara yako.
- Kupenda biashara unayofanya.
1. Nidhamu binafsi katika biashara.
Nidhamu ni nguzo muhimu sana katika biashara yoyote. Haijalishi ni kiasi gani unapata faida, haijalishi una mtaji mkubwa kiasi gani, bila kuwa na nidhamu binafsi ya kusimamia biashara hakika hauwezi kupiga hatua katika biashara. Lazima ujenge nidhamu katika maeneo haya: matumizi yako ya pesa, matumizi ya muda wako, nidhamu katika mipango yako. Ukikosa nidhamu binafsi katika biashara hautakuwa na muda maalumu wa kufungua au kufunga biashara, leo utapanga hivi kesho unabadili tena. Leo utauza hiki kesho hiki. Biashara ya namna hii lazima itakufa wala haitadumu.
2. Uthubutu wa kufanya mambo.
Bila kuthubutu kufanya huwezi kufanya, Stephen Saad, bilionea kutoka Afrika kusini anasema, " In life, you don't get anywhere or do anything you hope to without sort of sucrife " . Biashara inahitaji uthubutu kwa hali zote kufanya kile ulichopanga, thubutu kuuza bidhaa ulivyopanga, thubutu kubadili mfumo wa biashara, thubutu kukuza biashara yako kwa kuwekeza n. K. Hata mimi kuandika kitini hiki nimethubutu.
3. Uvumilivu mkubwa hasa biashara inapopitia changamoto.
Kila biashara ina changamoto zake. Hakuna biashara yoyote iwayo ambayo imenyooka pasi kupitia changamoto. Wapo watu ambao hutapeli na kudanganya watu eti biashara fulani ni rahisi na kwamba unatajirika mapema sana. Binafsi naamini huwa ni danganya toto, huwezi kusema unafanya biashara halafu muda mwingi umekaa tu, halafu unatajirika mapema. Kila biashara lazima ipitie changamoto mathalani : mzunguko mgumo ( transaction), kukosa wateja, kupata hasara muda mwingine, kupotelewa na bidhaa au hata pesa, bidhaa kubaribika au kuchakaa na kushuka thamani, mabadiliko ya fasheni pia mabadiliko ya sheria yanayopelekea kufungwa kwa matumizi ya bidhaa fulani. Haya ni magumu amabayo biashara inaweza kupitia, hivyo lazima uvumilivu uwepo katika mazingira kama haya.
4. Utambuzi wa hali ya juu kuhusu uendeshaji wa biashara yako.
Biashara nyingi zinakufa kutokana na kujua kutotambua namna biashara inavyoendelea. Kutojua kama unaendesha biashara kwa hasara, kuwa na usimamizi mbovu, kutotathmini muda ambao bidhaa inakaa. Haya yote hupelekea anguko la biashara yako. Katika uendeshaji wa biashara yako mambo haya ni muhimu ujue (a) mapato na matumizi (b) mtiririko wa mauzo (c) urasmishaji katika Mamlaka ya Mapato (d) leseni na vibali halali vya biashara husika.
5. Kujua namna ya kuongeza wateja wapya na kulinda wateja.
Biashara yoyote no mchezo wa wateja. Biashara ikikosa wateja lazima itakufa tu. Hivyo ni muhimu kujua namna ya kuongeza wateja wapya na kuwalinda ulionao wasiondoke. Jaribu kuongea na mteja ajisikie ni sehemu ya biashara yako, wasiliana kwa namna ambayo itamfanya mteja aipende huduma yako. Angalia mambo kadhaa hapa ambayo yatakusaidia kuongeza Wateja.
Boresha mawasiliano na mteja, tumia kadi ya mawasiliano ( business card)
Mfanye mteja aipende huduma yako kwa kumpunguzia bei na kumshawishi anunue zaidi.
Jenga ukaribu na mteja, ikiwezekana mpelekee huduma mteja alipo.
Jitahidi kujua majina ya wateja wako na kazi zao ili uwahudumia kadiri ya uhitaji wao.
Epuka kugombana na mteja. Ukimhudumia mteja moja vizuri atakuletea wateja zaidi.
6. Kujiwekea malengo katika biashara yako.
Malengo ni nguzo muhimu sana katika biashara. Pengine swali la msingi kupita yote ni kujiuliza unafanya biashara kwa lengo ( malengo ) gani? Je, unafanya biashara kwa kuwa rafiki yako ana biashara hiyo? Je, unafanya biashara ili kupanua mtaji? Au unafanya biashara ili kupata tu mahitaji yako kila siku yaani kwako biashara sio kwa ajili ya kupiga hatua fulani. Weka malengo katika biashara yako tena bainisha lini utafikia malengo hayo. Haya ni baadhi ya malengo unaweza kuijiwekea.
Uwe na malengo ya kupanua mtaji
Uwe na malengo ya kuboresha huduma kila siku.
Uwe na malengo ya kuwekeza katika miradi mbali mbali.
Uwe na malengo ya kutengeneza akiba nzuri.
7. Kuwa mbunifu na kutafuta kujifunza zaidi kuhusu biashara yako.
Ili biashara yako iendelee kusitawi ni sharti uwe mbunifu katika kuiendesha na pia upende kuijua zaidi biashara yako. Tafuta mtu makini na mbobevu wa biashara kama yako. Omba ushauri juu ya namna ya kuiendesha biashara. Kumbuka hata kama umeifanya biashara yako kwa miaka bado unahitajika kujifunza zaidi kila siku ili kuboresha biashara yako. Kila siku mambo yanabadilika hivyo lazima kujifunza kila siku.
8. Kupenda biashara unayofanya.
Unahitaji kuipenda biashara yako. Biashara yoyote ambayo huipendi utaiona kuwa ni mzigo, utaichukia, utaichoka na kutamani kuihama. Ili biashara ikue lazima mfanyabiashara husika aionee fahari biashara yake, awe na shauku ya kuifanya, atamani na kuamini moyoni mafanikio kupitia hiyo biashara. Usifanye biashara ambayo huipendi eti kwa sababu unataka kuganga njaa. Biashara ni kama taaluma, ukiwa mwalimu huku hupendi ualimu hiyo kazi utaiona kuwa ni mzigo, ukiwa Nesi huku hupendi kuhudumia wagonjwa itakuwa mzigo kwako, ukiwa mwanafunzi kuku hupendi kusoma huo ni mzigo, ukiwa mwanajeshi huku hupendi kushida dolia huo ni mzigo, ukiwa mkulima huku hupendi kulima huo ni mzigo. Penda kazi unayofanya kwa moyo, penda biashara unayofanya kwa moyo. Hakika ukipenda kwa moyo unachofanya utakifanya kwa ubora, kwa uzuri usiochakalika, kwa bidii isiyopimika.
Mwisho wa makala yangu, napenda kukutakia kila la kheri katika biashara yako. Mungu akubariki sana, akutie nguvu na imara ili ukatende kadiri ya mapenzi mema. Pia usisite kuwasiliana nami kwa kupitia blog hii www.hazinamaarifa.blogspot.com au barua pepe kwenda paulsonnghera@gmail.com.
HAZINA YA MAARIFA
Simu 0753-268271
E-mail paulsinnghera@gmail.com
P. O. Box 20,
Misungwi-Mwanza.
Comments
Post a Comment